#MALEZI BORA
UKUAJI BORA WA MWANAO:
Cheza na zungumza naye; maendeleo ya mtoto
wako huanza toka wakati wa mimba na hufanyika kwa haraka sana katika miaka
michache ya mwanzo ya maisha ya mtoto. Unaweza kufanya mengi kuchochea
maendeleo ya afya ya mtoto wako katika miaka hiyo ya mwanzo. Hiki ni kipindi
ambacho unaweza mjengea mwanao ujuzi ambao ni msingi muhimu kwa maisha yake
yote ya baadaye. Mwanao anakusikia na kujenga hisia akiwa tumboni. Gusa tumbo
lako kwa upendo, msemeshe na mwimbie mwanao ili aanze kutambua sauti yako na
kujenga upendo. Mwenzi wako pia anaweza kushika tumbo lako na kuongea na
mwanae.
AMEZALIWA
Mtoto wako kwa sasa anaona na kusikia,
mtazame machoni ukiwa unatabasamu, ongea naye kwa kumwita jina lake, ongea na
mwimbie kwa upole ili kujenga mahusiano naye. Hii inaweza kufanyika wakati
unamnyonyesha, mwogesha mtoto, unambembeleza au wakati mwingine wowote
unampomshika mtoto.
UTAMBUZI
Mtoto wako
anavutiwa na vitu vyenye rangi mbalimbali, muonyeshe vitu vya rangi mbalimbali
ili aweze kukuza uwezo wake wa kuona. Waweza tumia nguo zenye rangi mfano
‘kanga’ kupitisha kwenye macho ya mtoto.
Mwanao
anapenda kuchezea mikono na miguu yake, mlaze kwenye mkeka au kitanda ili
acheze kwa uhuru na kujenga misuli yake. Mguse au mmasaji mwanao kwa upole huku
ukimwimbia.
ISHARA
Mtoto wako
hulia kukuelezea mahitaji yake kama vile kunyonya, amejisaidia, anahisi joto.
Jifunze kutambua mahitaji hayo ili kuyatekeleza ipasavyo na kwa wakati. Usijali
kuhusu kuwa utamharibu mtoto wako kwa kumdekeza. Malezi chanya yatasaidia
kujenga mahusiano bora ya mwanao na pia kujiamini. Mwanao anaanza kulala na
tumbo na kugeuka na kufikia vitu vilivyowekwa karibu. Msogezee vitu vyenye
rangi ya kung’ara na sauti ili kumsaidia kushika na kuimarisha misuli. Unaweza
kutumia chekeche iliyotengenezwa, mpira mlaini na mwepesi au mwiko mdogo wa
mbao. Mwanao anapendelea kuweka vitu mdomoni. Mpatie mwanao vitu visafi,
visivyo na ncha kali au vidogo kama punje ili kuepusha kumkaba au maradhi.
KUONGEA
Mtoto wako
anaweza kutoa sauti ya kujirudia rudia kwa mfano ‘ba ba ba’, ‘da da da’ au ‘ma
ma ma’. Ongea naye kwa maneno kamili mfano ‘mama’ ‘baba’ ili kumrahisishia
kujifunza lugha. Pia mtajie mwanao vitu unavyoona, sikia au nusa kwenye
mazingira ya nyumbani. Mfano, ‘Mtazame baba yako/mama yako’ ‘Umemuona ng’ombe?’
Tumia sura na sauti yako kuonyesha hisia.
NAKILI
Mtoto wako
anazidi kutambua sura yako, akikuona huruka ruka na kutabasamu kwa furaha,
onesha upendo kwa kutabasamu, kucheka, kumsemesha na kumbeba ili kuimarisha
mahusiano na upendo. Mtoto anaanza kuzoea utaratibu wa kila siku unaomfanyia
mfano muda wa kuoga, kujisaidia na kulala. Msaidie kufuata utaratibu huo mfano
kufuata muda wa kulala, kuoga nk ili kumjenga kimwili na kiakili. Mtoto hujihisi
salama anapokuwa na mzazi au mlezi. Unapoondoka muage kwa upendo, kwa kumbusu,
kumpungia mkono na mhakikishie kuwa utarudi ili kumjengea uwezo wa kujiamini na
kutokuwa na hofu.
Mtoto
anaanza kuinuka, kukaa na kutambaa na pia uwezo wa utambuzi unaongezeka. Mpatie
vitu vya kuchezea vyenye maumbo, rangi na sauti tofauti tofauti ili aendelee
kukua kiakili na kimwili. Mfano chupa tupu za maji zilizowekwa mawe madogo ili
kutoa sauti, sufuria ndogo na mwiko ili kugonga nk. Ni muhimu kuhakikisha vifaa
anavyopewa mtoto na mazingira ni safi na salama ili kumwepusha mwanao na
hatari. Muweke mwanao mbali na moto au vitu vya moto, kamba, dawa au mafuta ya
taa. Muweke mwanao mbali na maji yenye kina mfano kisima, bwawa au ndoo.
KAZI NDOGO NDOGO NA
NYEPESI KABISA
Mtoto wako
anaweza kujifunza, mpe vitu anavyoweza kupanga au kuingiza ndani ya vingine,
mfano mikebe na vikombe; mruhusu akusaidie kupanga vitu, kama vile vibanio,
soksi kwa jozi au rangi, pia anaweza kuchora kutumia kalamu na karatasi ili
kumjengea misingi ya kujifunza. Mtoto wako anahitaji vitu vya kuchezea, sio
lazima vinunuliwe, unaweza kutengeneza mwenyewe kwa kutumia vifaa
vinavyopatikana kwenye mazingira yanayokuzunguka. Unaweza tengeneza mpira
kutumia vitambaa vya nguo, kamba au majani ya mgomba, unaweza tengeneza mdoli
kutumia nguo au majani ya mnazi. Mtoto wako anaweza kujifunza. Imba naye nyimbo
za vitendo kama vile “simama kaa”, “ruka ruka”, au nyimbo za viungo vya mwili
mfano ‘kichwa, mabega, magoti’ huku akionyesha viungo vyake ili kuendelea
kumjengea misingi ya kujifunza zaidi. Mpongeze mwanao kwa vitendo anavyofanya.
Mtoto wako anaweza kusimama, kutembea kwa kushika vitu/watu au mwenyewe. Mpatie
vifaa mfano baiskeli ya mbao ya kusukuma ili kumjengea uwezo zaidi. Pia unaweza
kutandika mkeka ili mtoto akianguka asiumie wakati anajaribu kutembea. Mpongeze
mwanao kwa kumpigia makofi na kumwimbia.
Mtoto wako
ana uwezo wa kusikiliza na kushika maneno machache, msimulie hadithi fupi, ili
kumpa uwezo wa kufikiria na kuhifadhi kumbukumbu ya maneno. Waweza kumsimulia
mwanao hadithi fupi au kusomea kitabu cha hadithi au picha. Pia unaweza
kumwambia mwanao akuambie hadithi yake au tukio lotote analokumbuka, sikiliza
ukitambua kuwa anaweza asiseme hadithi yote kwa makini na mpongeze. Mtoto wako
anatambua rangi na vitu mbalimbali, mtengenezee picha na vitu mbalimbali
kulingana na mazingira yenu mfano gari kutumia boksi au mdoli kutumia nguo na
muelekeze kuvitambua, kulinganisha na kutofautisha mfano vifaa vikubwa na
vidogo. Mtoto wako anaweza kuongea sentensi fupi yenye maneno mawili mpaka
matatu, msaidie ayatamke vizuri na kujua maana yake ili aweze kujieleza vizuri.
Mtoto wako
anapenda na anaweza kufanya vitu mwenyewe muelekeze afanye kwa usahihi, mfano
kula chakula na kuvaa nguo ili aweze kujitegemea. Pia mtoto wako anapenda
kusaidia kazi ndogondogo za nyumbani mfano, kufagia, kupanga vyakula toka
sokoni na nguo zilizofuliwa mpongeze na muelekeze ili kumpa moyo wa kuendelea
kujifunza.
BALEHE NA KUENDELEA
Wakati mtoto
wako ana hamu ya kujitegemea, pia katika umri huu mtoto anaweza kukasirika
kirahisi pale mambo yasipoenda sawa. Mfundishe mwanao aweze kufanya matendo
mazuri kwa kumpa upendo, kumwelesha kuhusu taratibu na kanuni za nyumbani. Mpe
mwanao upendo zaidi ya adhabu au kumgombeza. Kumkumbatia, kumbusu na kucheza
naye kutadhibitisha upendo kwa mwanao. Kumpongeza na kumfuatilia mwanao
kutamshawishi mwanao kufuata taratibu na kanuni zaidi ya kumpa adhabu. Mwanao
anaongeza udadisi na kujifunza kwa kuuliza maswali mara kwa mara. Mjibu mwanao
maswali yake kwa kumpa maelezo kwa kifupi.
Bakora na
kumfokea kwa makosa atakayoyarudia itapendeza zaidi.
Share,comment,like ili wengine wakumbuke na waelimike.
No comments:
Post a Comment