Waziri wa maliasili na utalii, Dk Hamisi Kigwangalla
ameitaka bodi ya utalii Tanzania (TTB) kuwekeza zaidi katika matumizi ya njia
za kisasa za mawasiliano na mbinu rahisi zenye gharama nafuu katika kutangaza
vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Aliyasema hayo Dodoma wakati akizindua rasmi bodi hiyo
ambayo Aprili, mwaka huu, Rais John Magufuli aliiongezea muda wa miaka mitatu.
Waziri Kigwangalla alisema kiu yake ni kuona sekta ya utalii
inakua na kuchangia pato la taifa, hivyo aliieleza bodi hiyo kuwa ina wajibu wa
kuendelea kubuni na kuongeza mbinu mpya za kutangaza utalii ili kuleta tija.
Alisema bodi hiyo inaweza kufanikiwa zaidi kama itafanya
kazi pamoja na wadau na taasisi nyingine za wizara ili kuongeza idadi ya
watalii wanaoitembelea Tanzania.
Aliweka msisitizo katika matumizi ya mifumo ya kisasa ya
mawasiliano ili kupanua wigo wa kutangaza vivutio vya utalii kuliko ilivyo
sasa.
Dk Kigwangalla aliipongeza bodi hiyo kwa kuendelea
kuhamasisha utalii nchini kwa kuja na kaulimbiu ya Tanzania Unforgettable
ambayo imekuwa chachu kwa taifa hasa katika kuitangaza sekta hiyo Kitaifa na
Kimataifa.
"Mnatakiwa kuwa na mkakati mahususi wa kukamata masoko
mapya ya watalii kutoka nje ya nchi kwa kufanya matangazo angalau mara tatu kwa
mwaka, ili kuvutia watalii wengi zaidi,"alisema.
Alizitaja nchi ambazo bodi inatakiwa kuweka mikakati
mahususi kuwa ni Marekani, Hispania, Urusi na nchi za Falme za Kiarabu zikiwemo
za Dubai na Oman ambazo watu wake wakiwemo wasomi, wafanyabiashara, wanamichezo
na walio maarufu wanapenda kwenda kupumzika kwa muda mrefu na kutumia fedha
nyingi kwa utalii.
No comments:
Post a Comment