Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
imetangaza mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 unaotaja
sifa, vigezo na utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mikopo ya elimu ya juu na
kuwasihi waombaji mikopo watarajiwa kuusoma kwa makini na kuuzingatia.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amewaambia
wanahabari jijini Dar es salaam kuwa lengo la kutoa mwongozo huo ni kuwawezesha
waombaji mikopo kuandaa nyaraka muhimu zinazotakiwa.
Kwa mujibu wa Badru, HESLB imetoa mwongozo huo kabla ya
kufungua mfumo wa maombi ya mkopo ili kuwawezesha waombaji mikopo watarajiwa
kuandaa nyaraka muhimu. Mfumo wa maombi kwa njia ya mtandao utafunguliwa Juni
15, 2019 na utafungwa Agosti 15, 2019.
Uzoefu na sababu za
kutoa mwongozo
“Uzoefu wetu unaonesha kuwa waombaji wengi hukimbilia kwenye
mtandao na kujaza fomu za maombi wakati mwingine bila kusoma mwongozo. Mwaka
huu tumetoa mwongozo huu kwanza ili wausome kwa wiki takribani mbili kabla ya
kuruhusiwa kuanza kujaza fomu kwa njia ya mtandao,” amesema Badru na kuongeza
kuwa katika mwaka 2018/2019, waombaji zaidi ya 9,000 kati ya 57,539 waliokuwa
na sifa za msingi walikosea kujaza fomu za maombi.
Ili kutatua tatizo hilo mwaka 2019/2020, Badru amesema HESLB
imetembelea shule za sekondari 81 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar
na kukutana na wanafunzi 27,489 ambao walielimishwa kuhusu sifa na utaratibu wa
kuomba mkopo kwa usahihi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema mwongozo huo unapatikana
katika lugha za kiingereza na kiswahili katika tovuti ya HESLB ambayo ni
www.heslb.go.tz
“Pamoja na mwongozo huo, pia tumeandaa kijitabu chenye
maswali na majibu yanayoelekeza namna ya kuomba mkopo kwa lugha ya kiswahili …
nacho pia kinapatikana kwenye tovuti yetu na tunawashauri wakisome,” amesema
Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Nyaraka muhimu za kuandaa
Waombaji wote wanatakiwa na vyeti vya kuzaliwa ambavyo
vimethibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Wakala wa
Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA). Aidha, kwa waombaji mikopo
ambao wazazi wao wamefariki dunia, watatakiwa kuwa na nakala za vyeti vya vifo
ambavyo vimethibitishwa na RITA au ZCSRA.
“Vilevile tunafahamu kuwa kuna wanafunzi waliofadhiliwa na
taasisi mbalimbali katika masomo yao ya sekondari au stashahada, hawa
wanatakiwa kuwa na barua kutoka katika taasisi hizo,” amesema Badru katika
mkutano huo uliohudhuriwa na Mkurugenzi wa Upangaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronika
Nyahende.
Kwa wanafunzi wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu,
Badru amesema wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu wao kutoka kwa
waganga wakuu wa wilaya au mikoa.
Maeneo muhimu
yaliyoboreshwa kwa 2019/2020
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo aligusia maeneo
muhimu yaliyoboreshwa katika utoaji mikopo kwa lengo la kuwafikia wanafunzi
wahitaji wengi zaidi.
“Baada ya kupokea maoni ya wadau, tumeongeza umri wa
waombaji mikopo kutoka miaka 33 hadi 35 na pia mwaka huu tutapokea maombi kwa
wanafunzi waliomaliza kidato cha sita au stashahada ndani ya miaka mitano
iliyopita … kabla ilikuwa miaka mitatu tu,” amesema Badru.
Malengo na bajeti
Katika mwaka wa masomo 2019/2020, Serikali kupitia HESLB
imepanga kutoa mikopo na ruzuku ya elimu ya juu yenye thamani ya TZS 450
bilioni kwa jumla ya wanafunzi 128,285. Kati ya hao, wanafunzi 45,000 watakuwa
wa mwaka wa kwanza. Mwaka huu 2018/2019, unaoelekea mwisho; jumla ya TZS 427.5
bilioni zilitolewa kwa jumla ya wanafunzi 123,000.
Dawati la huduma kwa
wateja
Pamoja na mwongozo uliotolewa, dawati la huduma kwa wateja
litakuwa wazi ili kutoa ufafanuzi pale utakapohitajika. Wateja wetu pia
wanaweza kupiga simu au kutuandikia barua pepe anuani na namba: Simu: 0736
665533 au 0738 66 55 33 au 022 5507910; Barua pepe: adcp@heslb.go.tz au
info@heslb.go.tz
No comments:
Post a Comment