MUME AMWACHA MKEWE KISA POMBE - waleo blog

Breaking

Wednesday 19 February 2020

MUME AMWACHA MKEWE KISA POMBE


#SHAIRI

1.Jamila nipe kalamu, na pepa pia sogeza,
   Niitoe yangu hamu, niwajuze na wa Mwanza,
   Pombe kwangu ni haramu, asije kunilemaza,
   Pombe sikutaki tena,pombe huzai mazuri.

2.Miaka kenda imepita, pombe nilikuabudu,
   Vilabuni kukufata,nilikuwa na Hamidu,
   Chochote sikukipata, wala Mungu kumwabudu,
   Pombe sikutaki tena, pombe huzai mazuri.
 
3.Wewe pombe mtu gani, ukipendwa hupendeki,
   Wakaribishwa nyumbani, na pesa lundo malaki,
   Bado wewe huthamini, maendeleo hutaki,
   Pombe sikutaki tena, pombe huzai mazuri.

4. wanirudisha nyumbani, kumbe wewe mnafiki,
   Nadia wangu mwandani, halali kucha mikiki,
   Kosa lake silioni,wataka nimtaliki,
   Pombe sikutaki tena,pombe  huzai mazuri.

5. Siku mbili zilopita,ulikuwa na jirani,
   Akadhani amepata, rafiki mwenye imani,
   Ndotoni akakuota, kumbe pombe ni mhuni,
   Pombe sikutaki tena, pombe kumbe mlaghai.

6. Jirani kumdanganya, eti wewe maarufu,
   Kumbe unamtekenya, apoteze maelfu,
   Umemwacha anahenya, wewe unakula ndafu,
   Pombe sikutaki  tena, pombe wewe mlaghai.

7. Walahi nakuapia, sikutaki asilani,
   Laini nakukatia, usije tena nyumbani,
   Unionapo kimbia, kajifiche vilabuni,
   Pombe sikutaki tena,pombe kumbe mlaghai.

8. Nane hapa ni tamati, kamwe sitaendelea,
   Pombe kwangu ni hayati, sitaki kumchekea,
   Wenzangu tujidhatiti, vipi ataendelea?
   Pombe sikutaki tena, pombe kumbe mlaghai.

No comments:

Post a Comment

Pages