Safari ya kufikia mafanikio siyo rahisi kama ambavyo wengi
wanafikiria. Ni safari ambayo inaweza kuwa ngumu sana hasa pale unapozungukwa
na jamii ambayo haioni kile unachokiona wewe.
Ili kufikia mafanikio ni muhimu sana wewe kuweka malengo na
mipango yako mapema kisha kuifanyia kazi bila kukata tamaa hata kama mambo
yatakuwa magumu kiasi gani.
Sisi sote tunataka na kutamani kuwa matajiri. Kwa wengi wetu, ni
ndoto tangu utotoni kwamba siku moja
tutakuwa matajiri. Ukweli ni kwamba, pamoja na kuwa ni kazi ngumu, lakini
tukiamua, tunaweza kujitengeneza sisi wenyewe kuwa mamilionea au mabilionea.
Lakini ukweli ni kwamba, kuwa tajiri siyo jambo la siku moja,
yaani kuamka na kujikuta wewe ni tajiri. Pia ni vigumu sana unapofikia uzee
ndiyo uanze kutafuta utajiri. Jambo hili huanza tangu mtu akiwa mdogo, akiwa na
uwezo wa kuunganisha bahati na nguvu zake za mwili na akili.
Zipo tafiti nyingi zinazoonesha kuwa, umri mzuri na usiokuwa na
changamoto nyingi za kujijenga kufikia utajiri mkubwa ni katika kipindi cha
miaka 20 hadi 30.
Huenda kipindi hiki ukawa ni mwanafunzi na ukawa na changamoto
nyingi za kimasomo ambazo zitakuzuia kufanya kitu kingine nje ya masomo kwa
hofu ya kukosa vyote.
Lakini kumbuka, hakuna njia ya moja kwa moja ya kujihakikishia
kuwa tajiri baadaye. Hapa ndipo linapokuja suala la kupata elimu sahihi ya
unachokitaka kisha linakuja suala la kupanga ni kuchagua na kwa wale wenye
uwezo mkubwa wa kiakili, wanaweza kuhimili yote kwa wakati mmoja. Yaani kusoma
na wakati huohuo kufanya biashara hata kama ni ndogondogo. Mtu huyu anaweza
kuanza na ‘vibiashara’ ambavyo wenzake watamwambia kuwa anapoteza muda bila
kujua anatengeneza mazingira ya kupata uzoefu wa kwenda kukabiliana na maisha
hasa atakapomaliza masomo na kukutana na tatizo kubwa la ajira.
Hapa nitajaribu kukupa njia saba (7) ambazo zaweza kukusaidia
kukujenga na kufikia utajiri mkubwa tangu ukiwa na umri mdogo wa kati ya miaka
20 hadi 30;
1: Amini huna muda mwingine
Unapokuwa na umri huo na ndoto yako ikawa ni siku moja kuwa
tajiri, anza mapema. Ujinga wa vijana wengi ni kuamini kuwa daima kuna muda wa
kutosha kwa kila kitu hivyo atafanya tu!
Vijana mara nyingi wanaamini kwamba kuanza biashara mapema au
kujenga ni mambo yanayokuja baadaye hivyo hujipumbaza kwa kuona kuwa bado muda
upo.
Kwa hiyo, kwa mantiki hii, hatua ya kwanza ni kuacha kusubiri
muda fulani ufike maana hautafika. Wengine wanakuwa tayari kuwekeza, lakini
wanaogopa suala la umri.
2: Hakuna uchawi
Matumizi ya neno ‘njia’ kwenye kichwa
cha mada hii ni kukuondoa kwenye mambo ya gizani. Nilitamani kutumia neno ‘siri’, lakini nikaliacha ili mtu
asiamini kwamba kuwa tajiri kuna nguvu za giza.
Hapa hakuna uchawi, ninachokufundisha ni ufumbuzi wa uhakika wa
kukufanya tajiri. Uchawi pekee ni kutumia kidogo unachopewa na mzazi au mlezi
na kuanza kufanya ujasiriamali hata kama ni wa shilingi elfu kumi wakati bado
ukiwa masomoni.
Katika mazingira kama hayo, jinsi unavyowekeza ni juu yako
kutokana na kile unachokipata kwa mjomba au shangazi anapokuaga wakati
unapochaguliwa kujiunga na ngazi fulani ya elimu.
Rafiki yangu usikubali kutumia chote unachopewa au kukipata hadi
kikaisha chote bila hata kuanzisha mradi wa kuuza mafuta ya taa mtaani au
maandazi kijijini au mtaani kwenu kupitia ndugu, rafiki au jamaa ambaye
utamwamini ambaye hakupata nafasi ya kuendelea na masomo au aliyemaliza masomo
awe msimamizi wako. Hapa usiwaze sana kuibiwa au kudhulumiwa kwani hilo laweza
kukutokea hata ukiwa unasimamia mwenyewe.
3: Kuwekeza ndani yako
Baada ya kujua kuwa, huna muda na hakuna uchawi katika mambo
haya, njia ya tatu ni kuanza mapema kadiri iwezekanavyo kuwekeza ndani yako.
Jambo moja muhimu wasilolijua wengi ni kwamba wewe ni rasilimali
kubwa ya kujitengenezea utajiri. Kuwekeza ndani yako wewe mwenyewe inamaanisha
kutumia muda wako mwingi zaidi kujijenga mno katika kupata ujuzi na
kujiunganisha na watu unaoamini wanaweza kukufikisha kwenye ndoto yako ya kuwa
tajiri.
Kwa wale waliopata bahati ya kwenda shule, wenye ujuzi na uzoefu
katika eneo fulani, wana fursa kubwa sana wanayoipata na kuwarahisishia njia
zao.
4: Panga bajeti
Kama nilivyosema awali, unaweza ukapata pesa kiasi fulani. Pesa
hiyo ni lazima iwe na bajeti la sivyo hutajua imepitia wapi, kufumba na
kufumbua utakuta huna hata kumi. Tumia kidogo na nyingine fanya uwekezaji.
Panga bajeti ya kina juu ya chochote unachokipata. Weka mipaka imara kwa
gharama zako ukizingatia pesa zikija huwa zinakutekenya ili uzitoe ziondoke
zake.
5: Epuka madeni
Kabla ya kuanza kutafuta na kuwekeza pesa, ni lazima ujilinde na
madeni ambayo yaweza kukutoa kwenye reli. Ukiacha mikopo ya masomo, ogopa sana
mikopo ya magari na vitu visivyokuwa vya lazima kwenye umri huo. Rafiki,
ukishatengeneza pesa, magari siyo ishu maana utaendesha ya kila aina, tena
yenye majina makubwa.
6: Usiogope kupoteza
Katika umri huo mdogo, usiogope kupoteza kwani unakuwa na miaka
mingi mbele yako kama Mungu atakujalia uhai. Usiogope kuwekeza kwenye maeneo
hatarishi zaidi. Fikiria, ukimaliza masomo, usiwaze kuajiriwa, anza biashara
yako mwenyewe. Vijana wengi wanaamini kwamba, ajira ndiyo ulinzi na usalama wa
maisha yao, lakini kwako iwe tofauti kwani nilishaeleza ulemavu wa kuajiriwa
uliyo mbaya.
7: Usitegemee ujuzi wa aina moja
Kuthubutu katika uwekezaji hata kama ni wa shilingi kumi ndiyo
msingi wa kuanza kufanya jambo. Lakini nakukumbusha tu kuwa, usitegemee ujuzi
wa aina moja. Jichanganye kwa kujiongeza kujua ujuzi mwingine na mwingine. Pia
usitegemee aina moja tu ya uwekezaji, badala yake jaribu kuanzisha vyanzo vingi
vya mapato, uzalishe mipangilio kadhaa ya uhifadhi kwa malengo na biashara
zako, tafuta fursa mpya kila mahali na kila kukicha.
Ninaamini kuwa, kwa kutumia njia hizi saba na Mungu akikujalia
uzima, utakuwa na uwezo wa kuanza kutengeneza utajiri bila kujali mahali ulipo.
No comments:
Post a Comment