#UJENZI
Nyumba ni
hitaji muhimu kwa watu wote. Kila mmoja anatamani na ana ndoto za kununua au
kujenga nyumba nzuri na ya kisasa.
Pamoja na
gharama kubwa za ujenzi wa nyumba bado watu wengi wamekuwa wakishindwa kupata
nyumba nzuri huku wakiwa tayari wamepoteza kiasi kikubwa cha pesa. Ni wazi kuwa
yapo makosa mbalimbali yanayosababisha hali hii yakiwemo yale ya ukosefu wa
elimu pamoja na uzembe wa aina mbalimbali.
Karibu
ufuatilie makala hii ili uweze kufahamu makosa 8 unayoweza kuyaepuka wakati wa
kujenga nyumba ili hatimaye uwe na nyumba bora.
1. KUTOZINGATIA KANUNI ZA KUNUNUA KIWANJA
Watu
wengi hawafahamu mambo muhimu ya kuzingatia wakati wanaponunua kiwanja. Hivyo
hujikuta wakiingia katika matatizo mbalimbali kama vile kuvunjiwa nyumba zao,
kujenga kwenye maeneo mabaya kama matindiga na mikondo ya maji. Ni muhimu
kuhakikisha mambo yafuatayo kabla na wakati wa kutafuta kiwanja cha kujenga
nyumba:
·
Kiwanja
hakina umiliki zaidi ya mtu mmoja
·
Kiwanja
hakina mgogoro wa kisheria
·
Kiwanja
hakiko kwenye hifadhi ya barabara au mazingira
·
Kiwanja
kinafaa kwa ujenzi (Siyo tindiga, eneo la magadi, eneo la maporomoko ya ardhi
au mkondo wa maji)
2. UCHAGUZI DUNI WA RAMANI
Mara nyingi mtu humwita fundi na kumwambia
kuwa “nataka unijengee nyumba ya vyumba vitatu”. Fundi anapouliza ramani
yako iko wapi wao husema we angalia tu nzuri alimradi iwe ya vyumba vitatu.
Hili ni kosa kubwa sana kwani husababisha watu wengi kujengewa nyumba ambazo
hawazipendi.
Ramani
nzuri kwa fundi inaweza isiwe nzuri kwako na familia yako. Zingatia uchaguzi wa
ramani kwa makini kulingana na wewe unavyopenda, hili litakufanya pia upende
nyumba itakayojengwa..
3. KUTOKUFANYA MAKADIRIO SAHIHI
Ni wazi
kuwa umeona nyumba nyingi zikianzwa lakini hazimaliziki. Hili kwa kiasi kikubwa
linatokana na kufanya makadirio na maandalizi duni kabla ya kuanza kujenga.
Ujenzi wa nyumba unahitaji maandalizi mazuri hasa kifedha. Ni muhimu kujiandaa
vyema kabla ya kuanza ujenzi ili usikwamie njiani.
Mambo
unayoweza kufanya:
·
Weka
makadirio ya gharama za ujenzi ili angalau uandae kiasi fulani cha pesa.
·
Nunua
baadhi ya vifaa kabla. Unaweza kununua mchanga, mawe, kokoto, nondo, mabati
n.k. Ili kupunguza matumizi ya pesa wakati wa ujenzi.
·
Weka
mipango ya kutunza mahitaji yako mengine ya pesa kabla ya kuanza ujenzi. Kwa
mfano ada za shule, kodi mbalimbali, chakula n.k.
·
Punguza
matumizi yasiyokuwa ya lazima kabla na wakati wa ujenzi. Ikumbukwe kuwa pesa
nyingi zitahitajika kwenye ujenzi.
4. KUTOKUBAINISHA MAHITAJI
Mahitaji
ya nyumba hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Hivyo ni vyema
ukabainisha mahitaji yako kwa nyumba husika. Nimeshuhudia watu wakijenga nyumba
na kuzivunja ua kuzifanyia marekebisho kila mwaka kutokana na kutobainisha
mahitaji yao mapema.
Kurekebisha
au kuvunja na kujenga upya nyumba yako kutakupotezea kiasi kikubwa sana cha
pesa. Kwa mfano wengi hurekebisha nyumba zao ili kuongeza vitu kama vile jiko,
choo na bafu, milango, madirisha n.k. ambavyo wangepanga mapema wangekuwa
wameviweka mwanzoni.
5. KUTOKUWAZA MBELENI
Ni vyema
kuwaza mbeleni kwani nyumba ni kitu utakachokitumia muda mrefu. Ni vyema
ukafahamu vitu na mahitaji utakayoyataka kwenye nyumba yako kwa siku za
mbeleni. Hili litakuwezesha kujenga nyumba utakayoitumia na kuifurahia kwa muda
mrefu zaidi.
Ni vyema
pia ukawaza kuweka miundombinu ya kisasa kama vile umeme, simu (intercom),
nyaya za televisheni, Kiyoyozi, na hata Data. Hata kama huna pesa za kuweka
mambo haya unaweza kubuni nyumba ambayo baadaye itaruhusu miundombinu hii.
6. KUTUMIA MAFUNDI DUNI
Wengi
hupenda kuokoa gharama kwa kutumia mafundi wenye uwezo mdogo ili wawalipe kwa
bei nafuu. Ni wazi kuwa rahisi inaumiza. Jiandae vyema kabla ya ujenzi ili
uweze kuitendea haki nyumba yako kwa kutumia mafundi bora wanaoimudu kazi yao
vyema. Kutumia mafundi bora kutakufanya kupata pia kazi yenye ubora.
7. KUPUUZA KANUNI MUHIMU ZA UJENZI
Ujenzi
una kanuni zake mbalimbali ambazo ni vyema zikazingatiwa. Kutokana na uelewa
mdogo, watu wengi hawazingatii kanuni muhimu za ujenzi kama vile kumwagilia
maji yakutosha pamoja na kujenga nyumba kulingana na muda.
Nimeshuhudia nyumba nyingi zikivunjika kutokana na
kujengwa haraka haraka bila kutoa muda wa kutosha kwa nyumba kukomaa na
kustahimili uzito. Pia nimeona watu wakipuuzia umuhimu wa kurowesha
sehemu iliyojegwa kwa maji mengi; ni muhimu kunyesha vyema eneo lililojengwa
kwani “uimara wa saruji ni maji”; unaweza kunyesha angalau
kwa siku saba asubuhi na jioni.
Nyumba
iliyoporomoka kutokana na kupuuza kanuni za ujenzi.
8. MATUMIZI YA VIFAA DUNI
Kama
nilivyoeleza katika maelezo yaliyotangulia, uhaba wa fedha huwafanya watu wengi
kufanya kazi duni. Hivi leo kuna vifaa mbalimbali vya ujenzi, lakini si vyote
ni bora. Kwa mfano, hakuna haja ya kununua kitasa kinachovunjika baada ya mwezi
au vigae vinavyofubaa. Kwa kufanya hivi utapoteza pesa nyingi kwa kununua vifaa
hivyo mara kwa mara. Jibane, jipange ufanye kitu cha uhakika.
No comments:
Post a Comment