Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, amewataka
wazazi nchini kutowaruhusu watoto wao kwenda kusherehekea Sikukuu ya Idd
ufukweni (Beach), huku akitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua kwa watakaokwenda
kusherehekea kwenye maeneo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Sheikh
Salum kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi, alisema imekuwa
kawaida kwa wazazi kuruhusu watoto kwenda kusherehekea sikukuu katika maeneo ya
ufukweni jambo ambalo linaweza kuchangia hata maambukizi ya Ukimwi.
Alisema ifike wakati mamlaka zinazohusika ikiwamo Jeshi la
Polisi kuwachukulia hatua washerehekeaji ambao watakuwa wanatumia usafiri wa
kukodi au binafsi kwenda katika maeneo hayo.
“Ninatoa wito kwa wazazi kuwazuia watoto wao kusherehekea
sikukuu kwa namna hii, pia ninawaomba polisi kutumia nafasi zao kuwakamata
wataokwenda kusherehekea ufukweni kwani huko ndiko wanakofanya maasi na kupoteza
maana nzima ya sikukuu hii,” alisema Sheikh Salum.
Pia alisema kwa mwaka huu sherehe za Idd zitafanyika katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wakati huohuo, Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata), limetangaza sherehe ya Idd el Fitr kitaifa
kwa mwaka 2019 itafanyika mkoani Tanga.
No comments:
Post a Comment