#MAHUSIANO
Siku hazisimami, daima zinasonga mbele kwa mbele. Mungu
ambaye ndiye mfalme wa kila kilichomo mbinguni na ardhini, anawezesha
mabadiliko ya kutisha ndani ya sayari ya dunia. Hakukosea Judith Wambura (Lady
Jaydee) alipoimba Siku Hazigandi.Kwa kila nukta tunayoivuka, mabadiliko
yanayotokea, neema zinazotufikia, mitihani inayotukabili, hatuna budi
kumshukuru yeye muweza wa yote. Hakika, mimi na wewe binadamu ni viumbe dhaifu,
kwa hiyo hatuna ujanja wa kufanya jambo lolote, isipokuwa kwa matakwa
yake.Tunayatazama mapenzi. Tunatoa mada nzuri ambazo lengo lake ni kukuzindua
wewe msomaji wangu ili ufanye tafakuri ya kina kuhusu uhusiano wako. Uziangalie
hatua zote ulizopita wewe na mpenzi wako kila siku. Naamini kuwa unajifunza na
unafanikiwa.Aidha, shabaha ya kila mada ni kutengeneza mwanzo wa kikomo cha
mateso kwenye mapenzi. Hii ni kukuweka sawa, kuangalia machungu ambayo kwa
maana moja au nyingine yanakukabili, hivyo ujipange upya, kurekebisha pale
ulipojikwaa kisha unafungua ukurasa mpya ambao hautakuumiza tena.
MIGOGORO, neno hili linamaanisha nini?Tafsiri: Migogoro ni
neno linalomaanisha wingi wa mgogoro ambalo linatafsiriwa kama hali ya
kutoafikiana baina ya pande mbili au zaidi. Pia inawezekana ikawa ni sura ya
fujo.Tunapoizungumzia migogoro, kwa hali yoyote ile haiepukiki. Na unapoitaja
katika uhusiano ni tatizo lisilo na mwenyewe. Maana ya kusema hivyo ni kuwa
kila mtu aliye ndani ya ndoa, uchumba au vinginevyo analia kwa staili yake.Sababu
ya kusema hivyo ni kwamba migogoro ni sehemu ya maisha ya kila mtu ambaye yupo
katika uhusiano. Kuna usemi wa Kiswahili kuwa vikombe ndani ya kabati
vinagongana, itakuwa watu wawili waliopitia makuzi tofauti?Hivyo basi, usemi
huo ndiyo unaothibitisha uwepo wa migogoro katika uhusiano wa kila mtu, ingawa
inatofautiana ukubwa kati ya mtu na mtu, kulingana na staili ya maisha ya
wahusika.Sambamba na hilo, jinsi ya kutatua migogoro ni kipimo kingine
kinachochangia utofauti kati ya uhusiano wa mtu mmoja hadi mwingine.
Inawezekana pia, hasira, busara na ustahimilivu ulionao ukawa chachu ya wewe
kutofautiana na jirani yako.Sababu hiyo, pia inayo matawi mengi, mojawapo ikiwa
kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi, au kufikia kipindi ambacho makosa yanakuwa
hayagawanyiki huku kila mmoja anakuwa hataki kukubali kosa.Kimsingi, silaha ya
kwanza inayoweza kuuokoa uhusiano wowote ule, ni kwa wapenzi wawili kukubali
kuwa na wajibu sawa katika kutafuta suluhu ya migogoro yao. Nafikiri hapo tuko
pamoja!Kikubwa ni kuelewa kuwa ni watu wawili ambao hufanya uhusiano wao uwe
wenye afya, pia ni katika idadi hiyo hiyo ambayo husababisha penzi lao lisifike
popote. Sababu ni ipi na utofauti huu unasababishwa na nini?Penzi ni fumbo
zito, ndiyo maana huwaunganisha hata wale watu wenye njozi zinazosigana.
Inawezekana kicheche akadumu kwenye penzi lake mpaka watu wakashangaa, wakati
mtu anayesadikiwa ni mtulivu akawa anahama uhusiano mmoja kwenda mwingine kila
siku.Hata hivyo, muhimu ni kujua mbinu ‘tekniki’ za kutatua migogoro. Kila mtu
ana wajibu wa kuufanya uhusiano wake kuwa wa kudumu, hivyo kwa kuzingatia hilo,
ndiyo maana nakuomba tukutane Jumatatu ijayo katika gazeti hili hili, ili
tupate kuendeleza maajabu ya XXLOVE.
No comments:
Post a Comment