UJAMAA NCHINI TANZANIA - waleo blog

Breaking

Wednesday, 1 April 2020

UJAMAA NCHINI TANZANIA


#Utawala

Ujamaa ni siasa iliyoanzishwa kwa misingi ya sera za baba wa taifa,mwalimu Julias  Kambarage Nyerere kwa maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi katika nchi ya Tanzania punde tu baada ya Tanganyika kupata uhuru kutoka kwa mwiingereza mwaka 1961.
Mwaka 1967 rais Nyerere alichapisha mwongozo wa maendeleo yake, ambao uliitwa azimio la Arusha, ambapo alionesha haja ya kuwa na mtindo wa kiafrika wa maendeleo na huo ukawa msingi wa Usoshalisti wa Afrika.

UJAMAA NI NINI?

Neno ujamaa linatokana na neno la  Kiarabu ,”JAMA-AA/JAMU-UU”ikiwa ni kwa wingi, yaani kwa Kiswahili likimaanisha “Mkusanyiko”/undugu/mfumo wa kiuchumi unoowezesha umma kumiliki njia kuu za kuzalisha mali na mgawanyo wa mapato kwa jamii yote.
 Mwalimu Nyerere alitumia Ujamaa kama msingi wa mradi wa maendeleo ya taifa. Aliitafsiri dhana ya Ujamaa kuwa mfumo wa usimamizi wa kisiasa na wa kiuchumi kwa namna mbalimbali zifuatazo:
1.   Kuweko kwa mfumo wa chama kimoja chini ya uongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) ili kusaidia katika kuimarisha mshikamano wa kujitegemea kwa Tanzania iliyokuwa  imejipatia uhuru.
2.   Ustawishaji wa usawa kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kuweko kwa demokrasia kuu; kukomesha ubaguzi kwa misingi ya hali ya mtu na kuzifanya sekta muhimu za uchumi kufikia taifa zima.
3.   Kupeleka uzalishaji katika vijiji, ambapo ulifanya uwezo wa uzalishaji wa aina zote kufanyika kwa pamoja.
4.   Kukuza kujitegemea kwa Tanzania kwa njia mbili: mabadiliko ya kiuchumi na mitazamo ya kiutamaduni. Kiuchumi, kila mtu angekifanyia kikundi chote kazi na kujifanyia yeye mwenyewe; kiutamaduni, ni lazima watanzania wajifunze kujikomboa kutoka kwenye utegemezi wa nchi za Ulaya. Kwake Nyerere, hii ilijumuisha watanzania kujifunza kujifanyia mambo yao wenyewe na kujifunza kuridhika na kile ambacho wangeweza kufikia kama nchi huru.
5.   Utekelezaji wa elimu bila malipo na ya lazima kwa Watanzania wote ili kuwahamasisha wananchi kuhusu kanuni za ujamaa.

Uongozi wa mwalimu Juliasi Nyerere uliivutia Tanzania macho na heshima ya kimataifa kutokana na msisitizo wake wa maadili kama msingi wa maamuzi ya siasa. Chini ya Nyerere Tanzania ilipiga hatua kubwa katika vipengele mbalimbali vya maendeleo; vifo vya watoto vilipungua kutoka 138 kwa 1000 waliozaliwa hai mwaka 1965 hadi 110 mwaka 1985; tarajio la kuishi lilipanda kutoka miaka 37 (1960) hadi 52 (1984). Uandikishaji wa wanafunzi katika shule za msingi ulipanda kutoka 25% (16% tu kwa watoto wa kike, mwaka 1960 hadi 72% (85% kwa watoto wa kike. Mwaka 1985, ingawa idadi ya wananchi ilikuwa inaongezeka kwa kasi lakini asilimia ya watu wazima waliojua kusoma na kuandika ilipanda kutoka 17% mwaka 1960 hadi 63% mwaka 1975  juu sana kuliko nchi nyingine za Afrika na  ikaendelea kupanda.

Hata hivyo ujamaa kama vile mipango mingine ya uzalishaji wa pamoja ulipunguza uzalishaji hata kutia shaka juu ya uwezo wake wa kustawisha uchumi.
Hatimaye sababu mbalimbali zilifanya ujamaa uonekane umeshindikana kiuchumi. Kati ya hizo, tatizo la kimataifa la mafuta miaka ya 1970, anguko la bei ya bidhaa zilizozalishwa nchini hasa kahawa na katani, utovu wa uwekezaji kutoka nje ya nchi na vita vya Uganda-Tanzania miaka 1978-1979 vilivyofvonza sana mtaji muhimu, na miaka miwili mfululizo ya ukame.
Kufikia mwaka 1985 ilikuwa wazi kwamba ujamaa ulishindwa kutoa Tanzania nje ya ufukara wake. Nyerere alitangaza kuwa atang'atuka asigombee tena urais katika uchaguzi wa mwaka huohuo.

Ujamaa ulivunjwa ingawa si kinadharia  mwaka 1985 wakati Nyerere alipomwachia mamlaka Ali Hassan Mwinyi aliyeingiza nchi katika taratibu za soko huria(RUKHSA).

Tukomee hapa kwa leo.Itaendelea……
Maoni na ushauri ni hapa
                                                        +255767611645
                                                        Adamgome96@gmail.com
                                                         +255715080716
       

No comments:

Post a Comment

Pages