Wanafunzi watatu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari
Makurugusi iliyopo Chato mkoani Geita, wamepoteza maisha kwa kuzama katika Ziwa
Victoria baada ya mtumbwi waliokuwa wamepanda kupinduka.
Walikuwa ziwani wakifanya mradi (project) ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya kuhitimu kidato cha nne.
Mradi wao ulikuwa unahusu ongezeko la watu na athari za
mazingira katika eneo la Mwalo wa Matofali Kibunda, Kata ya Makurugusi, ambao
waliuanza Mei mosi na walikuwa wawasilishe ripoti yao kesho.
Akitoa ufafanuzi juu ya tukio hilo, kamanda wa Polisi mkoani
Geita, Mponjoli Mwabulambo, aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Atha Gabriel
(19), Manyencha Faustin (18) na Masalu Hamis (22).
Kamanda Mwabulambo alisema wanafunzi watano wakiwa kwenye
mafunzo yao ya mradi, walitamani kutembelea mandhari ya ziwa hilo, wakaamua
kukodi mtumbwi ili kufanya utalii wa ndani.
Alisema walipanda mtumbwi ambao dereva alikuwa Daud Thomas
na wakati wakiwa umbali wa mita 120 kutoka ufukweni, mmoja wao, aliyejulikana
kama Samson Kano alivua nguo na kutumbukia majini kwa nia ya
kuogelea.
Kamanda Mwabulambo alisema kuwa mwanafunzi huyo alipotaka
kurudi katika mtumbwi, alivuta ukingo wa mtumbwi huo na ndipo ulipoegemea
upande huo na kupinduka.
“Mtumbwi ulipopinduka
wanafunzi wote walizama na kati yao watatu walizama kabisa, huku wengine wawili wakifanikiwa
kuogelea na kutoka,” alisema.
Kamanda Mponjoli aliwataja waliookolewa kuwa ni Abiana
Fitina (19) ambaye pia alikunywa maji mengi na hali yake sio nzuri na mwingine
ni Yohana Yamonda (19).
Alisema harakati za kuwaokoa zilifanyika chini ya uongozi wa mkuu wa wilaya ya Chato, Mtemi Msafiri, Mkuu wa polisi wa wilaya na wananchi ambazo
zilichukua siku nzima ya juzi hadi miili kupatikana saa 11 jioni.
Kamanda Mwabulambo aliwaonya wananchi watumiao vyombo vya
majini kuhakikisha wanafuata taratibu na kanuni za usafiri huo.
No comments:
Post a Comment