#KILIMO
Wataalamu wa afya
wanashauri ya kuwa, usikose angalau matunda mawili mezani wakati wa mlo.
Matunda yamesheheni madini mbalimbali, na yanafahamika kwa kiini
kizuri cha Vitamini.
Kuna matunda kama vile; machungwa,
ndizi, matufaha, maembe, maparachichi, mapapai, karakara na mapera, haya yakiwa
machache tu kuorodhesha.
Katika makala hii, tunaangazia tija za mapapai na namna ya
kuyapanda.
Tunda la papai lina Vitamini A, B, C, D na E, hivyo basi tunda
hili linaorodheshwa katika kundi la matunda na vyakula vyenye utajiri mkubwa wa
Vitamini.
Wataalamu wa afya ya tiba
lishe,wamekubaliana kwamba, mbegu za
mapapai hukabiliana na shida ya tumbo.
Hutibu udhaifu wa tumbo
kama vile kutosagika kwa chakula.
Wazazi hushauriwa kuwapa watoto wao mapapai kwa wingi, hasa
wakiwa wadogo kwa kuwa matunda haya huwawezesha kuenda haja bila matatizo.
Aidha, matunda haya hayana asidi yakilinganishwa na machungwa,
hivyo basi walio na shida ya asidi hupendekezwa kuyala kwa wingi.
Nchini Kenya, maeneo yanayojulikana kuyakuza kwa wingi ni Nyeri,
Embu, Meru na Kirinyaga. Yanastawi katika udongo tifutifu na udongo wa
kufinyanga.
Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya kilimo hasa matunda
anasema yanahitaji udongo wenye uchachu wa wastani, pH 6.0-7.0.
“Ninahimiza mkulima kujua asidi na alkalini ya udongo wa shamba
lake kabla ya kuanza kukuza mimea,” anashauri Bw Mwenda.
Kulinga naye ni kuwa ukuzaji wa mapapai hauna gharama ya juu.
Mdau huyu anasema miche ya mapapai huchukua muda wa miezi miwili na nusu katika
kitalu.
Upanzi
Mbegu za jinsia ya kiume na kike ni suala la kuzingatia, ambapo
asilimia 95-98 inafaa kuwa kike na iliyosalia iwe ya kiume. Bw Mwenda anasema
mbegu za mapapai huuzwa kulingana na jinsia.
Miche ikikaribia kuwa tayari kwa uhamisho, mkulima anashauriwa
aanze maandalizi ya shamba. Kipimo cha shimo moja hadi lingine kiwe na nafasi
ya mita 2.5, na kutoka laini moja ya shimo hadi nyingine iwe na kipimo sawa na
hicho.
Urefu wa shimo kuenda chini unategemea aina ya udongo na kimo
cha mche. Mwenda anasema udongo tifutifu unahitaji shimo lenye urefu wa futi 1
kuenda chini, na upana wa futi 1.5.
Anaendelea kueleza kwamba mashimo ya udongo wa kufinyanga yawe
na urefu wa nusu futi kuenda chini na upana wa kipimo sawa na hicho.
Mipapai inanogeshwa na mbolea hai. Udongo wa juu uchanganywe na
mbolea, mchanganyiko huo urejeshwe shimoni hadi karibu nusu futi. Catherine
Nyokabi, mtaalamu wa kilimo na mkulima wa mapapai Nyeri na Laikipia, anasema
miche ipandwe kisha imwagiliwe maji. “Nafasi iliyosalia ni ya nyasi za boji (mulching),
kwa minajili ya kuzuia uvukuzi wa maji hasa wakati wa jua kali,” anasema Bi
Nyokabi.
Miche inayopaswa kupandwa ni yenye urefu wa karibu futi moja.
Baada ya upanzi, mipapai itunzwe kwa maji na mbolea ya mifugo
ili kuinawirisha. Isitoshe, nafasi iliyoko kati ya mti wa matunda inaweza
kupandwa mimea yenye madini ya Nitrojini, kama vile maharagwe.
Bw Mwenda anasema ni nadra mapapai kuathiriwa na magonjwa. Hata
hivyo, magonjwa kama Pawpaw ring Virus na Bacterial
wilt hushuhudiwa iwapo mkulima hakabiliani na makwekwe shambani.
Mdudu aina ya Tiripsi ndio hushambulia mapaipai. Kukabiliana na
changamoto za magonjwa na wadudu, mkulima anahimizwa kupata ushauri kutoka kwa
wataalamu wa kilimo au katika maduka ya kuuza bidhaa za kilimo.
Mazao
Ekari moja inasitiri kati ya mipapai 800-900. Kwa msimu, mpapai
huzalisha zaidi ya kilo 40. Kilo moja sokoni inagharimu Zaidi ya Sh40, ingawa
inategemea msimu na maeneo. Ni muhimu kutaja kwamba mipapai huanza kuzalisha
matunda kuanzia mwaka wa pili baada ya upanzi.
Mbali na kuliwa, mapapai hutumika kuzalisha sharubati kwa
kuchanganya na matunda mengine kwa njia ya kupondaponda kutumia blenda.
No comments:
Post a Comment